Thursday, March 14, 2013

Udobi aliyeanza kupata Sh2,000 mpaka Sh 20,000 kwa siku




Na Joseph Zablon, Mwananchi 
Posted  Alhamisi,Marchi14  2013

Tatizo la ajira lina wagusa watu wengi hasa vijana. Wengi wanaangaika kutafuta ajira bila mafanikio huku wengi wakiwa ni wahitimu wa vyuo vikuu.
Kila mwaka vyuo vikuu nchini vinazalisha wataalamu wa kila aina, lakini wengi wamebaki mitaani kutokana na kukosa ajira.

 Kulingana na tafiti mbalimbali nchini kila mwaka kuna wastani wa wahitimu 1.2 milioni wanaomaliza masomo kutoka vyuo mbalimbali vya elimu ya juu na kati yao wanaoingia katika ajira ni 200,000 pekee.
 Idadi hiyo ni mbali ya wale ambao wanakatiza masomo kwa sababu mbalimbali na ambao wanahitimu ngazi ya vyeti katika vyuo ufundi na fani nyingine. Takwimu hizo zinabainisha kwamba kuna tatizo la ajira na ubunifu unatakiwa kukabiliana nalo.
Mbali na hayo kauli mbiu ya kuwataka vijana kujiajiri ambayo imekuwa ikitolewa na wanasiasa na watu  wengine sio jambo jipya kwa Watanzania wengi.
Mkazi wa Mtaa wa Midizini, Manzese jijini Dar es Salaam, Saleh Juma ‘Mabua’, dobi maarufu Mtaa wa Midizini, ni mmoja wa watu waliojiajiri, lakini akipitia milima na mabonde mpaka kufikia mafanikio.
Juma ameanza kazi hiyo miaka 10 iliyopita katika mtaa huo wa uswahilini ambako wakazi wake wengi wanaishi katika kipato kidogo, chini ya dola moja. Awali  Juma alikuwa akitumia pasi ya mkaa, meza, ndoo na mabeseni kwa ajili ya kufulia nguo za wateja  ambao wengi wao ni wapangaji katika nyumba za kulala wageni.
Hivi sasa anamiliki mashine ya kufulia, pasi ya umeme na pato limeongezeka kutoka Sh2,000 za awali mpaka Sh20,000.Mabua anasema siri kubwa ya mafanikio yake ni kuamua kujiajiri baada ya kumaliza elimu ya shule ya msingi.
 “Toka mwanzo wa maisha yangu baada ya kumaliza elimu ya msingi, niliiota kujiajiri na kazi iliyokuwa karibu yangu ilikuwa ya kufua na kupiga pasi nguo za wateja,” anasema.
Anasema kazi hiyo haikuwa rahisi kwani wakati mwingine alikuwa anayumba na hivyo kuacha kazi hiyo kwa muda na kurejea tena kuifanya.
Wakati dobi huyo akifanya hivyo mtangazaji wa siku nyingi wa Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD), Nassoro Nsekeli alimshauri aiheshimu kazi yake wala asiidharau kwa kuwa ilimsaidia kupata kipato.
“Yule mzee (Nsekeli) nilikuwa nazungumza naye sana na wakati wote linapofika suala la ajira, alinisisitizia kutafuta umaarufu kupitia kazi yangu,” anasema.
Anasema mwaka 2000 alianza kufanya kazi ya udobi kwa bidii na kuacha kazi nyingine na kwamba kadiri siku zilivyokuwa zinazidi kwenda, alipata mafanikio zaidi.
Dobi huyo anasema ametumia mapato yanayotokana na kazi hiyo kuboresha ofisi yake kwa  kununua mashine ya kufulia na pasi ya umeme.
“Nilijikuta nina akiba ya kama Sh1 milioni hivi na zaidi, fedha ambazo kulingana na utafiti wangu wa awali zilikuwa zinatosha kununua mashine ya kufulia, pasi ya umeme na kumudu gharama nyingine,hivyo sikufanya ajizi,” anasema.

Siri nyingine kubwa ya mafanikio yake anasema ni umakini na kuthamini  kazi za watu ambazo walikuwa wanampelekea.
 “Nilikuwa nafua, napiga pasi mwenyewe, nikihofia kutoa kibarua kwa wengine ambao pengine wangezifua isivyotakiwa au kupiga pasi hovyo kwani mwisho wa siku lawama zingerudi kwangu,” anasema.
Anasema siri nyingine ni umakini katika kutambua nguo za wateja jambo ambalo anajisifu kuwa analimudu vema na muda mwingi akiwa katika kazi yake hiyo hajafanya makosa ambayo yamefikia hatua ya kumgharimu.
“Sijawahi kukosea kiasi cha kusababisha nimlipe mteja fidia.
 “Sasa mambo ni tofauti sana,  angalau napumua kidogo kwani nimeanza kusahau adha ya kufua nguo kwa mikono na kuhangaika na kuwasha pasi na adha nyingine za namna hiyo ambazo zimesababisha nitumie muda mwingi na nguvu nyingi,” anasema Mabua.
Anasema uaminifu umesababisha watu kuheshimu kazi yake na wateja, marafiki na kipato kimeongezeka zaidi.
Wateja hawachukui nguo
Anasema baadhi ya wateja wamekuwa wakimuachia nguo baada ya kumpelekea ili azifue na kupiga pasi.
Anasema hali hiyo huwa inamuweka katika wakati mgumu inapotokea kwani anakuwa hajui mteja wake huyo kitu gani kimemtokea.

“Inapotokea hivyo nasubiri kwa muda fulani, mteja asipokuja natafuta utaratibu wa kuzitunza baada ya kuziondoa katika eneo langu la kazi,” anasema.
Wateja kutelekeza nguo zao kunachangiwa na sababu nyingi ikiwa ni pamoja na wengine wanasafiri kwenda mbali ghafla na kutokurudi kabisa.
“Mtu mwingine anakutwa na mauti, na ndugu zake hawana taarifa kuwa alipeleka nguo kwa dobi na wapo ambao wanapata ajali au dharura nyingine,” anasema.
Anasema nguo za namna hiyo baada ya muda anazigawa kwa watu wengine kwani zikaa muda mrefu zinaharibika.

No comments:

Post a Comment