Thursday, March 14, 2013

Pele: Hakuna mkato kwenye soka

"Soka barani Afrika mazingira yake yanafanana, hakuna mtoto wa waziri anayecheza soka, wala hakuna mtoto wa mwanasheria au mfanyakazi wa benki ambaye anacheza soka, soka inachezwa na watu wanaotoka kwenye familia duni na hilo ndiyo daraja la kuelekea maisha mazuri,"alisema Pele.
Mwananchi
Posted  Jumatatu, Novemba5  2012 


NYOTA wa zamani wa Ghana na Olympique Marseille, Abedi Pele amewaambia wachezaji chipukizi wa Tanzania kuwa hakuna njia ya mkato katika kutafuta mafanikio katika soka.

Pele, aliyeiongoza Marseille kutwaa ubingwa wa Ulaya mwaka 1992, huku akifunga moja ya mabao dhidi ya AC Milan ya Italia alisema hayo jana asubuhi wakati alipotembelea kituo cha kufundisha wachezaji watoto wa kuanzia umri wa miaka sita hadi 17.

Pele aliwaambia katika kufikia mafanikio hakuna njia ya mkato na aliwataka wafanye jitihada ili watimize ndoto zao ikiwa ni pamoja na timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 17 'Serengeti Boys' inahakikisha inafuzu kucheza Fainali za Afrika mwakani.

"Tunaona wachezaji wenye vipaji vikubwa duniani wakifanya jitihada kubwa ili waweze kucheza kwa kiwango cha juu, bila ya kufanya juhudi, kujituma na kudhamiria hauwezi kufanikiwa,"alisema Pele.

Alisema,"Wale wenye vipaji, lakini hawafanyi jitihada hawataendelea, wale wasiojaliwa kuwa na vipaji, lakini wanafanya jitihada, watakwenda mbele na kupata mafanikio," alisema nyota Pele ambaye ameletwa nchini na Shirikisho la Soka Kimataifa (Fifa) kuangalia shughuli mbalimbali za maendeleo ya mpira wa miguu nchini.

"Soka barani Afrika mazingira yake yanafanana, hakuna mtoto wa waziri anayecheza soka, wala hakuna mtoto wa mwanasheria au mfanyakazi wa benki ambaye anacheza soka, soka inachezwa na watu wanaotoka kwenye familia duni na hilo ndiyo daraja la kuelekea maisha mazuri,"alisema Pele.

Pele, ambaye jina lake halisi ni Abedi Ayew aliwataka wachezaji wa timu ya taifa ya vijana 'Serengeti Boys' kufanya kila wawezalo ili wafuzu kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika zitakazofanyika Morocco mwakani.

"Mkifuzu mtakuwa mmefungua milango ya mafanikio ya maisha yenu," alisema Pele.

Pele ameambatana na Mkurugenzi wa  Maendeleo wa Fifa kwa nchini za Kusini mwa Afrika, Ashford Mamelodi na mmoja wa viongozi wa Idara ya Mawasiliano ya Fifa, Emmanuel, ambapo  watakuwa nchini kwa siku tatu ili kupata taarifa za shughuli mbalimbali za maendeleo, zikiwamo za soka la watoto (grassroots), soka la vijana, soka la wanawake na miradi mingine ya maendeleo.

No comments:

Post a Comment