Wednesday, February 6, 2013

Vyuo vya ufundi stadi kichocheo muhimu cha maendeleo ya Taifa

Na Fred Ayazi, Mwananchi. February 5 2013

KILA mwaka, zaidi ya nusu ya wanafunzi wanaohitimu darasa la saba na kidato cha nne, hawapati fursa ya kuendelea na ngazi ya elimu iliyo mbele yao kwa sababu mbalimbali.
Mfano mzuri ni mwaka jana ambapo wanafunzi waliofanya mtihani wa kuhitimu darasa la saba walikuwa 983, 545, lakini waliofaulu ni 567,567. Hivyo wanafunzi 415,978 hawakufanikiwa kuendelea na masomo ya sekondari.
Katika kundi hili wamo watakaosomeshwa na wazazi, walezi ama wafadhili katika shule binafsi. Lakini kuna maelefu wengine watakwama kabisa kuendelea na elimu ya sekondari.
Kwa nchi masikini kama Tanzania, kuzalisha watu zaidi ya 500,000 kila mwaka ambao hawapati ujuzi wowote, ni kuongeza umaskini katika nchi ambayo hivi karibuni tulielezwa kuwa idadi ya watu wake imefika milioni 44.
Hili ni doa kubwa katika mchakato wa kuiletea nchi maendeleo. Makala haya yanauliza kwa mwenendo huu, ni lini Tanzania inaweza kuifikia nchi kama vile Korea Kusini ambayo mpaka mwaka 1961 ilipopata uhuru, viwango vya uchumi vya nchi mbili hizo vilikuwa vinalingana.
Naibu Spika wa Bunge la Korea Kusini, Park Byeong-Seug, anasema mwanzoni nchi yake ilikuwa kama Tanzania, na wala haikuwa na maliasili ambazo zingeweza kuikwamua. Kutokana na hali hiyo, anasema kuwa waliamua kuwekeza kwenye rasilimali watu na hiyo ndiyo siri ya mafanikio yao. “Korea hatukuwa na maliasili, tuliwekeza kwa watu. Kuwekeza kwenye akili ndiyo siri ya mafanikio yetu. Elimu ndiyo siri kubwa kama unataka kupata maendeleo,” anafafanua.
Tofauti na Korea Kusini, Tanzania imejaaliwa rasilimali za kila aina kama madini, wanyama, gesi, ardhi, misitu na nyingine nyingi, lakini bado wananchi wengi wanaishi katika maisha ya kifukara.

Ujenzi wa vyuo vya ufundi
Kwa baadhi ya watu kiwango hicho cha umaskini kingeweza kupungua endapo nchi ingekuwa na vyuo vingi vya ufundi stadi ambavyo kazi yake ingekuwa kuhakikisha kila mhitimu wa darasa la saba na kidato cha nne anayeshindwa kuendelea na masomo ya juu, anapatiwa stadi za kumwezesha kujitegemea.
Kwa kufanya hivi, vijana ambao sasa wanaonekana mitaani wakiwa hawana cha kufanya, wangepata ujuzi ambao ungewasaidia kujiajiri.
 Ili kudhihirisha kuwa hali ni mbaya upande wa elimu ya ufundi, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa, anasema uwezo wa kutoa mafunzo ya ufundi stadi nchini ni asilimia nane tu ya mahitaji halisi. “Wahitaji karibu 700,000 kila mwaka hawana mahali pa kwenda baada ya kuhitimu elimu ya msingi na sekondari, hali hii inachangia ukosefu wa ujuzi na ajira,” anasema. Kwa sasa anasema nchi ina vyuo 627 vya ufundi stadi, ambapo 27 ni vyuo vya Serikali na 600 vinamilikiwa na watu ama taasisi binafsi.

Kila mwaka, vyuo hivi vinakadiriwa kudahili wanafunzi 121,348, huku maelfu wengine wakikosa fursa. Kwa sababu hii, Dk Kawamba, anasema suluhisho la hali hiyo ni ujenzi wa vituo vya mafunzo ya ufundi stadi katika kila wilaya.
“Serikali ina mpango wa kujenga kituo cha mafunzo ya ufundi stadi katika wilaya zote 139 zilizopo nchini,” anasema. Hata hivyo, anaonyesha wasiwasi wa Serikali kuwa na fedha za kutosha kutekeleza mradi huo uliokuwa ukitajwa kwenye kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM).
 “Ni imani yetu kuwa, Serikali ya Korea itashirikiana na Tanzania kuhakikisha kuwa, mikoa yote mipya (Njombe, Katavi, Simiyu na Geita) pamoja na wilaya zote, zinakuwa na vyuo vya ufundi vya wilaya na mikoa,” anaeleza.
Itakumbukwa kuwa, mwaka 2005 Serikali ya Korea iliipa Tanzania mkopo wa dola za Marekani 18 milioni. Pamoja na mambo mengine, fedha hizo zilitumika kujenga vyuo vinne vya ufundi stadi katika Mikoa ya Lindi, Manyara na Pwani, mikoa ambayo mwanzo haikuwa na vyuo vya ufundi vya mikoa. Pia fedha hizo zilitumika kujenga Taasisi ya Teknolojia Habari na Mawasiliano. Taasisi hiyo iliyopo Kipawa mkoani Dar es Salaam, iko chini ya Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta).
Dk Kawambwa anasema kwamba, vyuo hivyo vipya vinne vitadahili wanafunzi 1,160 sawa na ongezeko la asilimia moja ya uwezo wa vyuo vyote nchini. “Vyuo hivi vinne, vimekuwa vya mfano kutokana na kuwa na vifaa bora na vya kisasa ikilinganishwa na vyuo vingine,” anasema.
Hata hivyo, anasema kuwa, pamoja na mkopo huo wa Korea, bado karakana 11 za vyuo hivyo hazijajengwa kutokana na ukosefu wa fedha. Anasema kwamba, ujenzi huo umekwama wakati ambapo Serikali ya Korea ilishaleta vifaa kwa ajili ya karakana hizo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Veta, Profesa Idriss Mshoro, pamoja na changamoto nyingine, anasema kuwa utoaji wa mafunzo yanayowiana na mabadiliko ya teknolojia ni changamoto inayowakabili. Mafunzo hayo wanayopata vijana wetu ambayo kila mzazi anataka yamkomboe mtoto wake kutokana na umasikini, Profesa Mshoro anasema hayakidhi mahitaji ya soko la ajira. Anasema kuwa, ili kukabiliana na changamoto hizo, wanatekeleza mpango wa uboreshaji wa vyuo, kutekeleza mitalaa inayowiana na mahitaji ya soko la ajira pamoja na kuwa na uhusiano wa karibu na viwanda pamoja na wadau wengine.

No comments:

Post a Comment