Friday, December 6, 2013

‘Nilianza na Sh1.5 milioni sasa napata Sh5 bilioni’


Na Fredy Azzah, Mwananchi

Posted  Alhamisi,Decemba5  2013  saa 15:50 PM

Kwa ufupi
Ukitaka kufanikiwa ni lazima uwe na nidhamu baada ya kuomba mikopo kutoka taasisi za fedha. Waswahili husema mvumilivu hula mbivu na penye nia pana njia. Hizi ni methali za Kiswahili ambazo watu wenye tabia ya kukata tamaa hawafiki mbali kibiashara.

Hali hii ni tofauti kwa Oliver Matemu, ambaye juhudi zake zimebadilisha maisha yake ndani ya miaka 15.
Matemu ni Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Kipipa Millers Limited, ambayo hivi karibuni iliibuka kinara kwenye shindano la kuzisaka kampuni ambazo zinazokua kwa kasi nchini.
Shindano hilo la Kampuni 100 (Top 100 Mid–Sized Companies), linaendeshwa na Kampuni ya Mwananchi Communications (MCL) na KPMG Tanzania, na kudhaminiwa na Benki ya NBC pamoja na Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).

Matemu anasema alianza biashara yake mwaka 1998 akiwa mkoani Mbeya na alikuwa akinunua unga wa mahindi kwenye mashine za watu na kusambaza kwenye maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na shule. “Biashara yetu tulianza na mtaji wa Sh1.5 milioni na nilikuwa nikinunua unga na kuuza kwenye taasisi kama shule, wakati mwingine tulikuwa tunasambaza pamoja na mchele.

Ilipofika mwaka 2005 nilichukua mkopo nikanunua mashine za kusaga na kukobua nafaka, pale Mbeya nilipoamia Mwanza nikahama na mashine zangu,” Anasema Matemu. Anasema kwa mwaka sasa anafanya biashara ya wastani wa Sh5 bilioni kutoka mtaji wa Sh1.5.

Nilianza na kilo 20
Mbali ya kusaga na kusambaza nafaka, pia alikuwa anasambaza vinywaji vya Kampuni ya Bia Tanzania (TBL).
Wakati huo mama huyo alikuwa akifanya biashara huku akiwa ni mwalimu wa shule ya sekondari.
“Nilikuwa nafanya shughuli zangu huku nikiendelea na kazi yangu ya ualimu, kazi ya ualimu niliifanya kwa miaka 12, baadaye nilipata tatizo la mkono wa kulia, nikaona siwezi kuendelea kufundisha nikaamua kuongeza nguvu kwenye biashara zangu,” anaeleza Matemu.

Mfanyabiashara huyo alianza biashara kwa kununua unga kilo 20 na kuusambaza, lakini sasa anasambaza tani 15 za unga kwa siku.
“Hii biashara ya msimu, wakati ukikuta tuna tenda kubwa tunasambaza mpaka tani 15 kwa siku,” anasema.
Anabainisha kwamba ushindi aliopata utamuweka kwenye nafasi nzuri zaidi ya kufanya biashara zake.

Kutokana na mafanikio hayo mkakati wake hivi sasa ni kuboresha zaidi mashine zake ili aendelee kufanya vyema zaidi. Anabainisha kwamba siri ya mafanikio yake ni kufanya kazi kwa bidii na kutokukata tamaa.
“Ukinikuta ofini kwangu wala huwezi kunijua, huwezi kujua ni nani bosi na ni nani mfanyakazi, navaa nguo za kufanyia kazi na ninafanya kazi pamoja na vijana wangu.

“Ukitaka kufanikiwa ni lazima uwe na bidii na uwe na nidhamu na mikopo, mimi kuna wakati nafanya kazi kuanzia saa 12:00 asubuhi mpaka 12:00 usiku, naenda mpaka vijijini mwenyewe kutafuta mazao,” anasema Matemu.

Sikuamini nimeshinda Top 100
Anasema siku ya kutangazwa kwa washindi wa shindano hilo hakutarajia kama angeweza kushika nafasi ya kwanza na mpaka sasa anaona kama anaota.

Anaeleza kwamba zilipotajwa kampuni kuanzia 100 mpaka ya 50 alijua kuwa amesahaulika kwani hakutarajia kuwa juu ya nafasi hizo. “Mpaka sasa hivi naona kama vile naota, lakini naamini kikubwa kilichotufanya tushike nafasi hii, ni namna ambavyo tunaandaa hesabu zetu,” anasema Matemu.
Venance Mushi kutoka Research Solutions Africa ambayo ni kampuni iliyofanya tathmini kwa kampuni zilizoshiriki shindano hilo kwa mwaka huu, amedokeza kwamba kwa mara ya kwanza alitaka kupuuza kwenda kwenye Kampuni ya Kipipa Millers Limited.

“Kuna kampuni nilikuwa nakwenda kuitembelea, njiani nikaona Kampuni ya Kipipa, nikataka kuipita, nikaenda kwanza kwenye ile niliyoilenga awali, nilipofika huko nikaambiwa kampuni hiyo ilishakufa.
Niliporudi nikasema ngoja nipite hapa Kipipa nione, kama unavyoona leo ndiyo hawa wameibuka washindi,” anasema Mushi.

Waziri wa Viwanda na Biashara Dk Abdallah Kigoda anasema serikali itaendelea kutengeza mazingira mazuri ya kufanya biashara ili wawekezaji wa nje na ndani watekeleze majukumu yao bila kikwazo.
Dk Kigoda anasema shindano la Top 100 Mid–Sized Companies linaimarika kila mwaka na lina nafasi kubwa ya kuimarisha uchumi kwa kampuni za Afrika Mashariki. “Ili kampuni hizo zifikie mafanikio waliyokusudia, serikali itajitahidi kuweka mazingira yatakayoziwezesha kufanya shughuli zake vizuri na kufanya uzalishaji kwa gharama nafuu,” anasema Dk Kigoda.

Washauriwa kuongeza juhudi
Anazitaka kampuni hizo zilizofanikiwa kuingia kwenye kundi la kampuni 100 bora kujitambua kuwa sasa wao ni washindi na hivyo wajitahidi kufanya shughuli zao kitaalamu zaidi.
“Kwa kiwango hiki mlichofikia nyie sasa ni washindi, mfanye kazi zenu kitaalamu zaidi,” anasema Dk Kigoda.

Anasema hivi sasa Tanzania imeshuka kwenye nchi zenye viwango vizuri vya kufanya biashara duniani na kusababisha baadhi ya wawekezaji kukimbia.

Anaeleza kwamba, suala hilo linaipa serikali changamoto ya kutengeneza mazingira bora na rafiki ili kuvutia wawekezaji kufanya shughuli zao kwa faida.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Zuhura Muro anasema kwa kushirikiana na KPMG, wanaendesha shindano hilo kwa sababu wanelewa ni njia muhimu ya kuhamasisha kampuni kufanya vizuri.

Anasema kampuni hizo ni muhimu kwa uchumi wa nchi na ustawi wake kwani kodi wanazolipa ndiyo zinazotumika kulipa askari, kutumika kwenye sekta ya afya na elimu.

Sasa ni wakati wetu wa kuinuka, lakini hatuwezi kuinuka bila kuwa na watu muhimu kama ninyi (kampuni 100 bora) kwani nyie ndio mnaotengeza ajira, nyie ni watu muhimu sana kwa uchumi wan chi hii,” anasema Muro.

Sasa mwaka wa tatu wa shindano hilo linaendelea kufanyika, mwaka 2011 Kampuni ya BQ Contractors ya Dar es Salaam ilishika nafasi ya kwanza huku mwaka 2012, Kampuni ya Helvetic Solar Contractors ya jijini Arusha ikichukua nafasi hiyo.

No comments:

Post a Comment