Friday, December 6, 2013

Alikuja Dar kama ‘house boy’ sasa ametajirika

Sindamka akiwa kazini. Picha na Elias Msuya

 
Na Elias Msuya, Mwananchi
Posted  Jumatano,Novemba27  2013  saa 16:33 PM

Tatizo la ajira kwa vijana limekuwa sugu hasa kwa nchi zinazoendelea kama Tanzania. Vijana wengi wamekuwa wakikimbia vijijini na kuingia mijini kila mwaka wakitafuta ajira.Wilfred Sindamka mwenyeji wa wilayani Kibondo Mkoa wa Kigoma, alihamia jijini Dar es Salaam mwaka 1995 akitokea mkoani Dodoma ili kujaribu kutimiza ndoto yake ya maisha. Endelea….

“Nilimaliza darasa la saba mwaka 1993 wilayani Urambo Mkoa wa Tabora ambako ndiko wazazi wangu wanaishi. Ila sikuchaguliwa kuendelea sekondari, hivyo nilifanya shughuli ndogondogo za biashara na kilimo.
“Biashara hizo zilinifikisha mkoani Dodoma mwaka 1994 ambapo nilifanya kazi ya kuuza maandazi, karanga na vinginevyo kwa kuajiriwa na mtu,” anasema Sindamka.
Anasema lengo la kuja Dar es Salaam lilikuwa ni kutafuta kazi na alipata msaada wa mwajiri wake aliyemwelekeza kwa ndugu yake anayeishi Magomeni Makuti jijini. “Nilifika Dar es Salaam mwaka 1995 kwa mzee mmoja anayeitwa Midasi aliyekuwa akifanya kazi Wizara ya Mambo ya Ndani. Kazi aliyonipatia ni kuwa ‘house boy’. Nilifanya kazi hiyo kwa zaidi ya mwaka mmoja Niliridhishwa na kazi kwa kuwa nilikuwa nakula, kunywa kuoga kama niko nyumbani, lakini sikuwahi kulipwa mshahara kama nilivyoahidiwa,” anasema na kuongeza:
“Hali ile haikunifurahisha, hivyo nilimuuliza mzee Midasi naye akaniambia nimweleze mkewe. Hata baada ya kumweleza, mama alinipiga chenga tu. Kwa hiyo nikaazimia kurudi nyumbani wilayani Urambo.”
Anasema baada ya yule mama kumpa nauli alirejea kwao Urambo lakini mambo yakazidi kumwendea kombo, hadi alipoamua kurejea Dar es Salaam mwaka 1998.
“Mama alinisikiliza, akauza mbegu zake za karanga kisha akanipa nauli. Hata hivyo safari hii sikutaka kurudia kwa mwajiri wangu wa kwanza ingawa pia sikujua nifikie wapi,” anasema.
Hata hivyo, anasema aliamua kwenda kwa rafiki yake anayeitwa Masanja ambaye walikutana siku za nyuma. “Tuliwahi kufika hadi Wizara ya Elimu ambapo nilikutana na ndugu niliyemfahamu ambaye aliniambia kuwa maeneo ya Mburahati kuna ndugu zetu nikawatafute na nilipofika niliwapata nikaishi kwao,” anasema.

Juhudi za kutafuta kazi
 Sindamka anasema aliamua kumtafuta rafiki yake Massanja aliyekuwa fundi ujenzi maeneo ya Kigamboni.
“Kuna kazi tulikuwa tukiifanya pale katika kampuni inayoitwa Lemas mtaa wa Samora. Niliendelea na kazi ya ujenzi kwa zaidi ya mwaka mmoja. Hata hivyo, anasema kuna wakati aliachana na kampuni hiyo na kujiunga na mafundi wengine kwenye kazi za ujenzi.
“Kuna siku nilikuwa nimebeba tofali sita kichwani napandisha juu ya ukuta maeneo ya Tabata, mara ngazi ikavunjika nikanguka chini na kuumia vibaya.”

“Nikaona kazi imekuwa ngumu na maisha yanazidi kuwa magumu. Ilifika mahali nilitamani tena kurudi Urambo ili nikalime, lakini nikajiuliza, mbona wenzangu wanaweza kazi na maisha yanakwenda?”
Baada ya hapo anasema alishauriwa na ndugu yake kufanya kazi kwenye kiwanda cha chuma ambako alilipwa mshahara wa Sh1,200 kwa siku, tofauti na kwenye ujenzi nilikolipwa Sh800 kwa siku.
“Niliifanya ile kazi lakini nikagundua kuwa ni ngumu kuliko hata ya ujenzi. Kulikuwa na moshi ambao ulinisababishia maumivu ya mwili. Kazi zenyewe hazikuwa na vifaa vya usalama, hivyo ilikuwa ni hatari tupu,” anasema.
Baada ya kuachana na hiyo kazi alipata rafiki mwingine aliyeitwa Hassan aliyekuwa na kazi ya kuchomelea vyuma na huo ndiyo ukawa mwanzo wa kujua kazi za vyuma.
“Licha ya ndugu zangu kunikataza kufanya kazi za kuchomelea, bado sikua na jinsi ila kurudi tena kwa Hassan ili nijifunze ile kazi,” anasimulia.
Kuna wakati walipata kazi kule Mbezi Beach waliyopewa na aliyekuwa mhandisi katika kiwanda cha UFI na alimwambia awe analala kwenye nyumba wanayoijenga naye akakubali.
“Nikiwa bado najifunza kazi hiyo, kuna siku mmoja wa mafundi alipata msiba wa baba yake mzazi, ikabidi aende Kibondo. Mara tena Hassan naye akapata msiba wa kaka yake, naye akaenda Tanga,” anasema na kuendelea:
“Nikawa nimebaki peke yangu na sijawahi kufanya kazi peke yangu. Ila mama Seni alishangaa kuona siendelei na kazi. Akanishauri niendelee ili aione kazi yangu.  “Siku iliyofuata nikatengeneza dirisha moja na nusu. Yule mama aliporudi akauliza, ‘hili dirisha umetengeneza wewe?’ nikamwambia ndiyo. Akauliza tena, ‘sasa mbona wewe ndiye fundi kuliko Hassan?’ nikakataa,” anasimulia.
Anasema hali hiyo ilimpa moyo na kumfanya aendelee na kazi kwa bidii hadi aliporudi mwalimu wake, Hassan.
“Hassan aliporudi, Mama Seni akamuuliza mbona mwenzako anafanya kazi vizuri zaidi? Yeye akapinga kuwa siyo mimi. Baadaye Hassan akaniuliza, ‘kumbe na wewe ni fundi, mbona husemi, au unadhani hatutakulipa?’ mimi niliendelea kusisitiza kuwa bado najifunza kutoka kwake,” anasema.

Jaribio la pili
Baada ya kazi ile kwisha alirudi kwenye kazi ya ujenzi ambako kulikuwa na kazi ya kuchomelea milango ya chuma na huko alikutana na rafiki mwingine anayeitwa Kilua. Anasema Kilua ndiye aliyemwelekeza mbinu zaidi za ufundi na kupatana na wateja. “Kuna wakati nilipata tena kazi nyingine Mbezi Beach. Kuna mtu alikuwa anaitwa Mchachu. Baada ya kufika kwenye kazi, Mchachu aliniambia kuwa hiyo kazi itatolewa kwa majaribio. Mtatengeneza sampuli atakayefanikiwa ndiye atapata kazi,” anasema na kuongeza:
“Mimi nilimchukua Hassan na tulikuta tena mafundi wengine wawili. Nilimchukua yeye kwa sababu niliona kama nitakosa hiyo kazi aipate yeye.
“Mke wa Mchachu alikuwa na mchoro kutoka Uganda ndiyo tulitakiwa tuutengeneze. Baada ya kufanya hilo jaribio, mafundi wote walichemka hata mwalimu wangu Hassan, kazi yangu ndiyo ilishinda.”
Anasema baada ya kushinda hilo jaribio, alitakiwa alete vyeti vya shule ambavyo hata hivyo hakuwa navyo. “Niliamua kudanganya ili nipewe ile kazi, hivyo wakaniambia nilete vyeti vyangu. Hata hivyo yule Mchachu alinipa tu ile kazi kwa kuniamini, wala hakudai tena vyeti. Huo ndiyo ukawa mwanzo wa mafanikio yangu,” anasema.
Baada ya kupata mafanikio, anasema aliamua kufungua karakana yake rasmi mwaka 2004 maeneo ya Mburahati karibu na uwanja wa Kifa. Katika karakana hiyo anasaidiana na vijana watano wanaopata ujira wao baada ya kazi.

Mafanikio
Wilfred Sindamka aliyezaliwa mwaka 1976 wilayani Kibondo anasema amepata mafanikio makubwa kupitia kazi yake hiyo. “Nimepata mafanikio makubwa, kwanza nimejenga nyumba yangu kule Majohe Gongo la Mboto, nimeanzisha saluni ya wanaume, nina gari la kutembelea na daladala. Nimeoa na nina watoto wawili. Namshukuru Mungu kwa mafanikio haya,” anasema na kuongeza:

“Kwa sasa kwenye karakana yangu ninatengeneza bidhaa za vyuma na aluminiamu. Natengeneza madirisha, milango, vitanda na vifaa vya ndani. Biashara ni nzuri kwa kuwa bidhaa za chuma kwa sasa zinakubalika zaidi.”
Anawashauri vijana kutokuchagua kazi, kwani kuwa na mafanikio siyo lazima uwe na elimu kubwa au upate mtaji mkubwa, bali ni kuwa na nia na utayari wa kufanya kazi. 

Tatizo la ajira nchini
Kwa mujibu wa Integrated Labour Force Survey, hadi mwaka 2006, asilimia 11.7 ya Watanzania wenye sifa ya kufanya kazi hawakuwa na ajira. Kati yao wanawake ni asilimia 12.6 huku wanaume wakiwa asilimia 10.7.

No comments:

Post a Comment